Monday, April 17, 2017

Mfumuko wa bei waongezeka


MFUMUKO wa bei wa Taifa kwa mwezi Machi, 2017, umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.4 kutoka asilimia 5.5 mwezi Februari, 2017.

Kuongezeka kwa mfumuko huo kunamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Machi, 2017 umeongezeka ikilinganishwa na kasi ya upandaji ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia Februari, 2017.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, gahirisi za bei zimeongezeka hadi 108.44 Machi 2017 kutoka 101.93 Machi 2016.

Taarifa hiyo inaonesha kwamba mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi Machi, 2017 umeongezeka hadi asilimia 11.0 kutoka asilimia 8.7 ilivyokuwa Februari, 2017.

Mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwaka kwa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani kwa Machi, 2017 umeongezeka hadi asilimia 11.7 kutoka asilimia 9.3 Februari, 2017 huku badiliko la fahirisi za bei kwa bidhaa zisizo za vyakula likiwa limebaki kuwa asilimia 3.6 Machi, 2017 kama ilivyokuwa Februari, 2017.

Aidha, mfumuko wa bei ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa Machi, 2017 umebaki kuwa asilimi 2.2 kama ilivyokuwa Februari 2017.

Taarifa hiyo ilisema fahirisi inayotumika kukokotoa aina hiyo ya mfumuko wa bei, haijumuishi vyakula vinavyoliwa nyumbani na migahawani, vinywaji baridi, petroli, dizeli, gesi ya kupikia, mafuta ya taa, mkaa, kuni na umeme.

No comments:

Post a Comment