Monday, April 17, 2017
Vita Vikuu vya Dunia vinakaribia? Juma la wasiwasi kuhusu Marekani na Korea Kaskazini
Ukafuatilia matukio, mijadala na ujumbe katika mitandao ya kijamii, unaweza kudhani Vita Vikuu vya Tatu vya Dunia vinakaribia.
Rais wa Marekani Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un wamekuwa wakijibizana vikali kuhusu mpango wa Korea Kaskazini kuendelea kustawisha silaha za nyuklia na pia kufanyia majaribio makombora, jambo ambalo taifa hilo haliruhusiwi na Umoja wa Mataifa.
Marekani ilituma kundi la meli zake za kivita karibu na Korea Kaskazini, jambo ambalo liliikera Korea Kaskazini.
Trump aionya tena Korea Kaskazini
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili haujakuwa mzuri tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Hata hivyo wiki iliyopita uhasama ulizidi na kufikia kiwango cha juu kuliko awali.
Jumatatu - Meli za kivita za Marekani
Rais Trump aliagiza kundi la meli za kivita za Marekani pamoja na meli moja yenye uwezo wa kubeba ndege na pia kutumiwa na ndege hizo kupaa na kutua, zielekee upande wa Korea Kaskazini.
Trump apuuzilia mbali mpango wa Korea Kaskazini
Taifa hilo limetekeleza majaribio kadha ya silaha za nyuklia na hilo halijaifurahisha Marekani.
Rais Trump alisema Marekani imejiandaa kuchukua hatua kivyake, bila usaidizi wa China, kukabiliana na tishio la nyuklia kutoka kwa Korea Kaskazini.
Jumanne - Kim amjibu Trump
Kim Jong-Un hakufurahishwa na hayo na alimjibu vikali Bw Trump.
Korea Kaskazini yamtaja Trump kwa mara ya kwanza
Trump apuuzilia mbali mpango wa Korea Kaskazini
Wizara yake ya mambo ya nje ilinukuliwa ikisema hatua hiyo ya Marekani ni ya "kipumbavu" na ikaahidi kujilinda "kwa nguvu zote za kivita."
China, ambao ni mshirika wa karibu zaidi wa Korea Kaskazini, walionya kwamba wataingilia kati na kutoa adhabu kali zaidi za kifedha kwa Korea Kaskazini iwapo taifa hilo lingefanya majaribio zaidi ya makombora.
Jumatano - China yazungumza
Vyombo vya habari vya China vilisema rais wa taifa hilo alimpigia Rais Trump kutuliza hali.
Marekani huenda isizuie makombora ya Korea
Rais Trump mwenyewe aliandika kwenye Twitter kwamba alikuwa amewasiliana na Rais Xi Jinping.
Bw Xi alidaiwa kumwambia Trump kwamba anataka amani na utahibiti eneo hilo na kwamba anaunga mkono pia juhudi za kumaliza silaha za nyuklia katika rasi ya Korea.
Alhamisi- Gwaride la wanajeshi
Korea Kaskazini ilizindua mpango wake mpya wa ujenzi wa nyumba za makazi na biashara mjini Pyongyang.
Ulionekana kuwa mpango wa kawaida tu, lakini ilikuwa pia fursa ya taifa hilo kuonyesha nguvu zake.
Waandishi wa habari wa mashirika ya kigeni walialikwa kushuhudia wanajeshi wakifanya gwaride na kutembea kwenye barabara za mji huo.
Donald Trump hakufurahishwa na hilo.
Aliandika tena kwente Twitter kwamba Marekani iko tayari kukabiliana na Korea Kaskazini.
Ijumaa- Onyo la China
China ilitahadharisha kwamba mzozo mkubwa kati ya Marekani na Korea Kaskazini "unaweza kutokea wakati wowote".
Ilizionya nchi zote mbili kukoma kurushiana vitisho, na kusema hakuwezi kuwa na mshindi katika vita.
Hayo yakijiri, Korea Kaskazini ilikuwa inakamilisha maandalizi ya gwaride kubwa na maonyesho ya kijeshi Jumamosi.
Jumamosi - Vifaru barabarani
Korea Kaskazini iliadhimisha miaka 105 tangu kuzaliwa kwa mwanzilishi wa taifa hilo Kim Il-sung.
Vifaru zilitolewa barabara za Pyongyang. Serikali ya Korea Kaskazini pia ilionyesha hadharani kwa mara ya kwanza makombora yanayoweza kuruka kutoka bara moja hadi jingine, na pia makombora ya masafa marefu yanayoweza kurushwa kutoka kwenye nyambizi.
Maafisa wa serikali ya Korea Kaskazini waliionya Marekani dhidi ya kuchukua hatua zozote, wakisema nchi hiyo iko tayari kwa vita.
Walisema watajibu kwa "mashambulio ya nyuklia".
Marekani: Hatutaivumilia tena Korea Kaskazini
Hayo yakijiri, Makamu wa Rais Mike Pence alielekea Korea Kusini kujadiliana na washirika wa Marekani kuhusu njia bora zaidi za kukabiliana na Korea Kaskazini.
Jumapili - Jaribio la makombora
Marekani ilidai kwamba Korea Kaskazini ilijaribu kurusha kombora, lakini likalipuka sekunde chache baada ya kupaa angani.
Inasadikika kwamba lilikuwa kombora la masafa marefu, ambalo hupaa juu anagani kwanza na ambalo huelekezwa, lakini baadaye huanguka hadi pahali ambapo panalengwa kutokana na mvuto wa dunia.
Umoja wa Mataifa umeipiga marufuku Korea Kaskazini kufanya majaribio kama hayo.
Rais Trump atachukua hatua gani?
Ni yeye mwenyewe pekee ajuaye jibu - au labda mwenyewe binafsi amekanganyikiwa!
Labels:
Kiswahili
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment