Monday, April 17, 2017

Muhongo ahimiza elimu kukuza uchumi


MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewaomba wananchi kuweka nia kubwa katika sekta ya elimu ili kukuza uchumi wa familia na Taifa.

Akizungumza katika vijiji vya Bugoji, Muhoji, Chumwi Mgango na Bwai katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa alisema bila kuwapatia elimu bora watoto, hali ya baadaye ya familia nyingi na hata taifa itakuwa shakani.

‘’Elimu ndio suala la msingi katika kupatia msingi bora wa elimu mtoto ili hapo baadaye aweze kulinufaisha Taifa. Katika masuala yote toeni kipaumbele katika elimu, afya na kilimo ambavyo ndio vya msingi na hapo,” alisema Muhongo.

Aidha, amewataka wananchi kuacha kulalamika na badala yake waongeze bidii katika utendaji wa shughuli za maendeleo, ikiwemo kilimo ili kuweza kuondokana na matatizo mbalimbali ya maisha.

Akizungumzia juu ya mradi wa maji aliwataka madiwani kusimamia suala la maji kwa kuhakikisha kwamba wanaliwekea kipaumbele kwenye vikao vyao ili kumuwia rahisi yeye kulibeba.

“…ndugu zangu mkitaka miradi iwe na uwezo na isiyo na uwezo ni lazima maombi yenu yawe rasmi na kuwa rasmi ni lazima madiwani wayajadili kwenye vikao vyao katika halmashauri,’’ alisema.

Kuhusu upungufu wa chakula, alisema wakati umefika kwa wananchi kuacha kutegemea mvua katika kilimo na kuanza cha umwagiliaji.

Naye Katibu wa Mbunge wa jimbo hilo, Ramadhan Juma alisema Profesa Muhongo amekwishaleta vifaa vya ujenzi ambapo jumla ya mifuko ya saruji ipatayo 1,269 na mabati 5,120 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule za msingi 111 na sekondari 20 ambapo mgawanyo wa saruji katika ukanda wa Bukwaya shule 13, kati shule 18, ukanda wa Mugango 13 kati ya 24, ukanda Majita 40 kati ya shule 69.

No comments:

Post a Comment