Monday, April 17, 2017
POLISI WANASA MTANDAO WA WEZI WA BAJAJI
Na ABDALLAH AMIRI,
JESHI la Polisi wilayani Igunga limenasa mtandao wa wezi wa bajaji ambao wamekuwa wakipora na kusababisha mauaji ya madereva wake kwa mwaka 2016 na mwaka 2017.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamisi Selemani Issa alisema katika uchunguzi wa kina wamenaswa watu watutu ambao walikuwa wakijihusisha na matukio ya mauaji wa madereva wa bajaji na kuzipora.
Alisema tangu kuibuka matukio ya wizi wa bajaji mwaka jana, polisi walikuwa wakiendelea uchunguzi kwa miezi tisa na juzi waliwakamata watuhumiwa watatu ambao ni vinara wa matukio ya wizi huo na mauaji.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Safari Anthoni (25), Safari Kija (22) ambao walikuwa madereva wa bajaji na John Emmanuel (30), wote wakiwa wakazi wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
“Tuliwakamata watu hawa baada ya uchunguzi wa miezi tisa, tumewakamata huko Kahama mkoani Shinyanga na katika uchunguzi tumebaini kuwa ndiyo waliojihusisha na mauaji ya waendesha bajaji watatu wa Kata ya Igunga mjini,” alisema.
Alisema baada ya kukamatwa watuhumiwa hao walifanya upekuzi majumbani kwao na kukuta wakiwa na bajaji tano, kati yake tatu ni za madereva wa bajaji waliouawa mwaka jana.
Bajaji tatu zilizotambuliwa ni zile zilizokuwa zikiendeshwa na Alex Okungu (30) aliyetekwa na kuuawa Agosti 16 mwaka jana, Songa Juma (24) aliyeuawa Desemba 10 mwaka jana na Maduhu Dwisha (35) aliyeuawa Machi 2 mwaka huu.
Polisi pia walikamata simu moja na kitambulisho, mali ya marehemu Maduhu Dwisha aliyeuawa Machi 2, mwaka huu na watuhumiwa walikiri kuhusika na matukio hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo alipongeza polisi kwa kufanikisha kupatikana kwa bajaji zilizoibiwa pamoja na watuhumiwa.
Alisema matukio hayo yalikuwa yakisikitisha na kuwafanya wananchi kuilalamikia serikali.
Mwaipopo alisema kutokana na matukio hayo kushamiri, aliagiza bajaji zote mwisho wa kuendesha shughuli zake iwe saa 1:00 usiku.
Labels:
Kiswahili
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment